ASILIMIA 96 YA WATU WANAOISHI NA MAMBUKIZI YA VVU NCHINI WANAJUA HALI ZAO-WAZIRI MKUU MAJALIWA

ASILIMIA 96 YA WATU WANAOISHI NA MAMBUKIZI YA VVU NCHINI WANAJUA HALI ZAO-WAZIRI MKUU MAJALIWA

Na,Saleh Lujuo-Dodoma.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema asilimia 96 ya watu wanaoishi na mambukizi ya VVU wanajua hali zao ambapo asilimia 98 ya wanaojua hali zao wapo kwenye tiba ya ARV na kati yao asilimia 97 wameweza kufubaza wingi wa virusi kwenye damu. 

Kauli hiyo ya Waziri Mkuu Majaliwa ameitoa leo Jijini Dodoma alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Mdahalo wa Kitaifa Juu ya Kuimarisha Ubia Baina ya Serikali, Wadau na Jamii kwa  Uendelevu wa Mafanikio ya  Mwitikio wa UKIMWI nchini ambapo amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umewezesha Taifa kuvuka malengo ya kupambana na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) ya 95-95-95 yaliyopangwa kufikiwa mwaka 2025.

"Serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji na mifumo endelevu ya upatikanaji rasilimali fedha kwa ajili ya afua mbalimbali za UKIMWI ikiwa ni pamoja na Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (AIDS Trust Fund) na mipango mbalimbali katika ngazi ya Halmashauri na Taifa kwa ujumla ili malengo ya kutokomeza ugonjwa huo yaweze kufikiwa". amesema Majaliwa.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Wizara ya Afya kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI hadi sasa imeweza kusambaza vifaa vya mtu kujipima mwenyewe maambukizi ya Virusi vya UKIMWI zaidi ya Mil. 1.6 kuanzia Mwaka 2021 nchini Tanzania. 

"Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kuongeza nguvu za kusambaza vifaa hivyo vya watu kujipima wenyewe Virusi vya UKIMWI ili kuweza kutambua hali zao wenyewe na kwa haraka kuhusu ugonjwa huo". amesisitiza Waziri Ummy.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu) Mhe.Jenista Mhagama amewataka Wanaume kuacha tabia ya kutumia wake zao kama kipimo cha kugundua hali zao.

"wanaume walio wengi wanawatuma wake zao wakapime ndio watumie vipimo vile". amesema Mhagama.

Awali Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoshi na VVU (NACOPHA) Bi.Leticia Mourice ameishukuru Serikali,Wabia na Wadau mbalimbali Kwa kuendelea kuwawezesha watu wanaoishi na VVU kupata dawa na huduma zingine.

Kilele cha Mdahalo wa Kitaifa Juu ya Kuimarisha Ubia Baina ya Serikali, Wadau na Jamii kwa  Uendelevu wa Mafanikio ya  Mwitikio wa UKIMWI nchini umeongozwa na kauli mbiu isemayo "imarisha ubia na ushiriki wa jamii kwa mwitikio endelevu wa Ukimwi Tanzania".

Post a Comment

Previous Post Next Post