MHE. JENISTA AWATAKA WANANCHI KATA YA MTYANGIMBOLE KUMCHAGUA MGOMBEA UDIWANI KUTOKA CCM.


MHE. JENISTA AWATAKA WANANCHI KATA YA MTYANGIMBOLE  KUMCHAGUA  MGOMBEA UDIWANI KUTOKA CCM.

Na,Mwandishi wetu-Songea

WANANCHI  wa Kata ya Mtyangimbole, Kijiji cha IKalangiro kilichopo Wilaya ya Songea Vijijini wametakiwa kutofanya makosa katika marudio ya uchaguzi mdogo wa  Udiwani katika Kata hiyo utakaofanyika Septemba 19 mwaka huu na kuombwa kumchagua mgombea anayetokana na Chama cha Mapinduzi, Twahibu Diwani Ngonyani.

Kauli hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Peramiho  Mhe. Jenista Mhagama wakati akizindua kampeni hizo  katika Jimbo la Mdaba mkoani Ruvuma ambapo alikutana na viongozi wa Chama pamoja wanachama wa CCM Kata.

Amesema kuwa, chama cha Mapinduzi kimewaletea mgombea sahihi ambaye atawatumikia wananchi na kushirikiana na Serikali  kutatua kero zao ili kuwaletea maendeleo kulingana na kasi ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Wananchi mnawajibu wa kuhakikisha mnachagua mgombea anayetoka na CCM katika uchaguzi huu wa marudio ili kukamilisha mafiga matatu na kunufaika na chama chenu chenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo," alisema Mhe. Jenista.

Aidha Mbunge huyo amesema, Ilani inayotekelezwa kwa sasa ni ya Chama cha Mapinduzi na kuwataka kumchagua Twahibu Diwani Ngonyani  ili aweze kuisimamia Ilani hiyo kwa vitendo akisema kuwa, jukumu la chama cha Mapinduzi ni kuleta maendeleo na kuwataka kukikopesha imani chama hicho kwa kumchagua mgombea wake nacho kitawalipa maendeleo.

“Serikali imejipanga kutatua  kero za maji na katika huduma za afya kuna mikakati ya ujenzi wa vituo vya afya kwa lengo la kuwapungiza adha wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma muhimu hali inayorudisha nyuma maendeleo,” Ameeleza Mhe. Jenista

Katika hatua nyingine Mbunge huyo amewataka wakinamama kuhakikisha wanawahimiza vijana na kinababa kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kumchagua mgombea anayetokana na CCM akieleza kuwa ni nia njema ya Serikali kuhakikisha inaboresha miundo mbinu ya barabara, upatikanaji wa mbolea kwa wakulima kwa bei nafuu ili kulima kilimo chenye tija.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Songea Vijijini Bw. Thomas Masolwa amewahimiza kumchagua Twahibu kwa ajili ya maendeleo yao ni siyo wagombea wengine kutokana na uzoefu wake ndani ya Chama hivyo atakuwa msaada mkubwa katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hao.

Naye  Mgombea wa Udiwani katika Kata ya Mtyangimbole Bw. Twahibu Diwani Ngonyani  akinadi sera zake ameahidi kushirikiana na wananchi wa Kata hiyo pindi watakapomchagua  kwa  kumpa ushindi wa kishindo.


Post a Comment

Previous Post Next Post