ZAIDI YA DOLA ZA MAREKANI MILLIONI 1 KUFADHILI TAFITI MBALIMBALI ZENYE MSISITIZO WA MASHIRIKIANO KATI YA VYUO VIKUU NA WADAU NCHINI
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),imeidhinisha miradi miwili yenye jumla ya Shilingi Milioni 240 kwa ajili ya kufanya utafiti ili kubaini sababu ya wanafunzi kufeli katika somo la hesabu.
Mchakato wa mradi huo umekamilika na katika mwaka huu wa fedha wa 2023/2024,unaenda kwenye utekelezaji.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 na mwelekeo wa vipaumbele kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 Jijini Dodoma,Mkurugenzi wa Tume hiyo Dokta Amos Nungu amesema pia wameidhinisha miradi 7 ya mapinduzi ya nne ya viwanda yenye thamani ya zaidi ya Bilioni moja.
"Serikali ilifadhili miradi ya utafiti kupitia COSTECH, baadhi ya miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na Tume inafanya ufuatiliaji wa miradi inayohusu kuboresha maabara za utafiti kwa ukarabati na ununuzi wa vifaa vya kisasa ikiwemo, Maabara ya Utafiti wa Baharini katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar mradi ambao tayari ulishakamilika". amesema Dkt. Nungu.
Dokta Nungu amesema COSTECH pia inawaibua na kwenda nao pamoja wabunifu mbalimbali kubwa ni kuweka mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa rasilimali fedha, sera na miongozo stahiki, mashirikiano, miundombinu na kuhakikisha mchango wa utafiti na ubunifu unaleta manufaa kwa Taifa.
"COSTECH inaendelea kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini kwa kuanzisha au kutoa usaidizi kwa vituo mbalimbali vya ubunifu (intemediaries) ili kuwafikia na kuwahuduma wabunifu kiurahisi". amesema Dkt. Nungu.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amewahimiza vijana wabunifu kuendelea kujitokeza ili COSTECH wawaelekeze cha kufanya.
"Katika kuratibu Utafiti na Ubunifu, COSTECH inaendelea kufanya kazi na wadau mbalimbali, kubwa ikiwa ni kufanikisha kuweka mazingira wezeshi kwa wabunifu ili kuhakikisha mchango wa utafiti na ubunifu unaleta manufaa kwa taifa". amesema Msigwa.
Moja ya jukumu la COSTECH ni kuratibu, kuendeleza na kuhawilisha teknolojia na ubunifu ambapo katika majukumu na vipaumbele vya Tume kwa mwaka wa fedha 2023/2024,wamepanga kukamilisha zoezi la ufadhili wa pamoja miradi ya utafiti wa Mabaraza ya utafiti duniani.
Tags:
Habari