TAASISI ZA UMMA ONGEZENI MATUMIZI YA TEHAMA KATIKA UENDESHAJI WA SHUGHULI ZENU- SIMBACHAWENE

TAASISI ZA UMMA ONGEZENI MATUMIZI YA TEHAMA KATIKA UENDESHAJI WA SHUGHULI ZENU- SIMBACHAWENE

Na,Saleh Lujuo-Dodoma

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene, amezindua mfumo wa kielektroniki wa kukusanya,kuchakata na kutunza kumbukumbu za kesi za jinai na tovuti ya ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambapo amezitaka taaissi za umma kuongeza matumizi ya TEHAMA katika uendeshaji wa shughuli zao.

Uwanzishwaji wa mfumo huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa Januari 31,mwaka huu wakati  akizindua Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini,ambapo alielekeza umuhimu wa uwepo wa mfumo Jumuishi wa Haki Jinai na Mifumo kusomana.

Akikabidhi mfumo huo leo jijini Dodoma waziri Simbachawene amesema matumizi ya TEAHAMA yataongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

"mpaka sasa zaidi ya kesi za jinai 17,411 zimesajiliwa katika katika mfumo huo ambapo kati ya kesi hizo kesi 7,361 zimeshafika mwisho na kutolewa hukumu na kesi 1050 zipo katika hatua mbalimbali za maamuzi". amesema Simbachawene.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Pauline Gekul amesema wao kama serikali dhamira yao ni kuona haki zote zinatolewa kwa wakati,hivyo ana imani mfumo huo utakuwa chachu ya kufanikisha hilo.

"haki ni suala muhimu sana na inapaswa itolewe kwa wakati na hivyo kupitia mifumo ya TEHAMA tunataka kuhakikisha haki zinatolewa kwa wakati". amesema Gekul

Naye Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Marry Matondo amewataka wataalam wa mfumo kuendelea kufanya utafiti ili kubaini changamoto zitakazojitokeza katika utekelezaji wa mfumo huo. 

Naibu Katibu Mkuu wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Exvery Daud amewataka watumishi kubadilika ili mifumo ilete tija.

Mkurugenzi wa Mashtaka Sylivester Mwakitalu amesema wataitumia mifumo hiyo kikamilifu ili itoe matokeo tarajiwa na kwa wakati.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA),Benedict Ndomba amesema lengo la mfumo huo ni kurahisiha upatikanaji wa taarifa sahihi zinazohusu uendeshaji wa mashtaka na kuratibu shughuli zinazofanywa na ofisi ya waendesha mashtaka ambazo ni kufungua na kusimamia uendeshaji wa kesi za jina nchini. 

Mfumo huo umejengwa na wataalam wa e-GA kwa kushirikiana na wataalamu wa TEHAMA kutoka Ofisi ya Mashtaka ambapo imesanifu na kujenga na kusimamia uendeshaji wa mfumo huo kupitia mifumo hiyo ambapo mpaka sasa tayari ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Jeshi la Polisi na Mahakama zimeshaunganishwa na mfumo huo.

Post a Comment

Previous Post Next Post