MATUMIZI YA VIPIMO VILIVYOHAKIKIWA KUPITIA WAKALA WA VIPIMO NI MUHIMU SANA-BI.KAHWA
Na,Saleh Lujuo-Dodoma.
Wakala wa vipimo Tanzania(WMA), imefanikiwa kuhakiki dira za maji 420,497 zinazotumiwa na Mamlaka mbalimbali za maji nchini ili kuondosha malalamiko ya wateja kupunjwa maji ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020/2025.
WMA imeanza kufanya uhakiki wa mita za umeme ikiwa ni kuendeleza jitihada za serikali za kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini lengo likiwa ni kuhakikisha Serikali inapata tozo iliyo sahihi kulingana na umeme uliosambazwa na mteja aweze kulipa kiasi sahihi kulingana na kiasi cha umeme alichopokea.
Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Stella Kahwa akingumzia utekelezaji wa majukumu ya wakala huo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2023/2024,leo Jijini Dodoma amesema Uhakiki wa dira hizo ni sehemu ya mambo ya msingi yanayochangia katika utekelezaji wa ilani ya CCM kwa kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inaendelea kuimarishwa na kuwafikia zaidi ya asilimia 85 ya wakazi wa vijijini na zaidi ya asilimia 95 kwa mijini ifikapo mwaka 2025.
"Wakala wa Vipimo inaahidi kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa Weledi na ufanisi kwa kuendelea kusimamia Sheria ya Vipimo sura 340 kwa kusaidia na kufanya kazi sambasamba na wadau wa sekta mbalimbali kama vile Mafuta, Madini, Usafirishaji, Kilimo ili kuhakikisha sekta zote zinakuwa na mchango mkubwa kwenye kuongeza pato la Taifa na ukuaji wa uchumi". amesema Kahwa.
Aidha amesema katika mwaka 2022/2023, WMA imehakiki mizani 4254 ya mazao ya kimkakati ikiwa Pamba ni 1566, Korosho 2286 na Kahawa 402.
" kuhakikisha Kilimo kinaendelea kuwa nguzo muhimu katika kuchochea uchumi wa nchi, Wakala wa Vipimo imeendelea kufanya uhakiki wa vipimo vinavyotumika katika kilimo ambavyo kwa sehemu kubwa ni mizani".amesema Kahwa.
Kwa upande wake Msemaji mkuu wa Serikali Gerson Msigwa ametoa wito kwa wananchi kushirikiana katika kudhibiti vitendo vya ukiukaji wa sheria ya vipimo na hivyo kusababisha mali za wakulima kupotea.
Wakala wa Vipimo WMA imeanzishwa mwaka 2002 lengo likiwa ni kuboresha huduma zilizokuwa zikitolewa na kupunguza gharama za kiutendaji kutoka mfuko mkuu wa serikali.