VIJANA 1000 KUNUFAIKA NA MRADI WA WAJIBIKA SCHOLARSHIP
Na,Mwandishi wetu-Dodoma.
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imetiliana saini mkataba na Benki ya NBC kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo vya Mamlaka ya Mafunzo na Elimu ya Ufundi(VETA) kupitia mradi wa wajibika Scholarship ambapo watatoa sh.milioni 100 zitakazonufaisha vijana 1000.
Kufuatia hatua hiyo Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa.Adolf Mkenda amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuunda timu Maalum ambayo utapitia na kuangalia fani ambayo inawigo mpana wa ajira.
Profesa.Mkenda ametoa maagizo hayo leoJulai 20,2023 jijini Dodoma, wakati wa hafla hiyo ya utiliaji saini baina ya Serikali ya Benki hiyo ya NBC.
Amesema pamoja na fani hizo walizochagua ambazo ni Ushonaji, useremala, Ufundi mechanical, ujenzi, pia iundwe timu maalum ambavyo itachangia fani moja itakayofundishwa ndani ya miaka 2 hadi mitatu ili kuleta ufanisi na kukuza soko la ajira kwa vijana hao.
"Mimi napendekeza iwe fani ya ushonaji na mitindo, kwa mfano nguo aina ya suti zinaagizwa kutoka nje ya nchi Kwa gharama kubwa na ni vazi ambalo linakubalika, hapa nchini wapo mafundi ambao wanakuja wanachukua vipimo wanapeleka nguo kushona nje ya nchi na gharama ni kubwa mana wateja wanalipa kwa dola,"amesema Prof.Mkenda.
Waziri huyo amesema wakipata wataalam katika eneo hilo ambalo lina wigo mpana wa ajira, watafanya vizuri na watapata fedha nyingi ambapo amewahakikishia uwazi katika matumizi ya fedha hizo kama wao walivyoomba na kwamba watakuwa huru kufanya ukaguzi wakati wowote watakapohitaji kufanya hivyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) Theobald Sabi amesema uwepo wa changamoto ya soko la ajira ni suala la kidunia na vijana wengi wa Tanzania wanahangaika kutafuta ajira, kupitia changamoto hiyo NBC imeona umuhimu wa kuviwesha vyuo vya VETA nchini kutoa elimu zinazotoa ajira Kwa vijana.
"Leo NBC inaungana na Serikali rasmi katika kuzindua ufadhili wa kuwasomesha wanafunzi wa VETA, kwa kuanzia NBC watawasomesha vijana 1000 katika vituo mbalimbali vya VETA nchini Kwa ufadhili wa milioni 100 Kwa kuanzia,"amesema Sabi
Amesema wanalenga kufadhili katika fani za ushonaji, mechanical, fundi ujezi na useremala, ambapo NBC itawaandikisha kwenye NBC business Class na kuwafungulia akaunti Maalum iitwayo NBC KUWANASI, ambapo wataweka Fedha na kutoa bila Makato yeyote na kupitia hapo wataunganishwa na fulsa za kifedha kama mikopo ili kuendeleza shughuli zao.
Mkurugenzi huyo amesema mkopo wanaotoa utaratibiwa na wizara na VETA, Benki inasisitiza kuwa mshirika wa Serikali katika kuendeleza elimu nchini.
Naye Kaimu Mkurugenzi VETA, Anthony Kasore, ameishukuru NBC huku akiwathibitishia kuwa watahakikisha vijana wa kitanzania wanaenda kupata ujuzi.
"Katika hili nipende kumshukuru Rais Samia ambaye anahitaji kuona vijana wakipata ujuzi wa mafunzo ya amali hapa nchini, tumepokea Fedha hizo Kwa ajili ya kwenda kutekeleza ujuzi ambao vijana wengi wanahitaji, vijana wengi wanahitaji ajira lakini wanakosa ujuzi,"amesema.