RC SENYAMULE AJIPANGA KUMALIZA MIGOGORO YA ARDHI MKOA WA DODOMA.
Na Saleh Lujuo-Dodoma.
BAADA ya jiji la Dodoma kutajwa kuwa kinara wa migogoro ya ardhi nchini mkoa umezindua mkakati maalum wa kushughulikia tatizo hilo utakao tekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja ukihusisha wataalam wa wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, amebainisha hayo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mkakati wa kushughulikia tatizo la migogoro ya ardhi katika jiji la Dodoma.
Amesema tangu kutangazwa rasmi kwa mpango wa serikali kuhamishia shughuli zake makao makuu ya nchi Julai 25, 2016, jiji la Dodoma limeendelea kukua kwa kasi kubwa na kuvutia fursa mbalimbali za uwekezaji kwenye sekta zote muhimu.
Amesema sekta hizo ni pamoja na huduma za kijamii, kiuchumi, biashara, ujenzi na uwekezaji wa miundombinu msingi.
“Kwa mujibu wa makisio ya mwaka 2022 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Jiji la Dodoma linakadiriwa kuwa na wakazi takribani 765,179 ambao ni sawa na ongezeko la asilimia 16.2 la idadi ya wakazi wote waliokuwepo mwaka 2016”amesema
Aidha, Senyamule amesema ongezeko hilo limesababisha uwepo wa mahitaji makubwa ya ardhi hususan la viwanja kwa ajili ya kukidhi matumizi ya shughuli za ofisi mbalimbali za umma na binafsi sambamba na biashara mpya zinazofunguliwa.
“Kimsingi halmashauri ya jiji la Dodoma kama ilivyo kwa halmashauri nyingine hapa nchini kwa sasa ni moja ya halmashauri zinazokabiliwa na kero za migogoro mingi ya ardhi,”amesisitiza
Amesema kwa kuzingatia hilo kumekuwa na jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikichuliwa na halmashauri ofisi ya mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa, kamishna wa ardhi mkoa pamoja na wizara ya ardhi na vyombo vingine vya utatuzi wa migogoro katika kuipatia ufumbuzi.
Kadhalika, amesema kwa muda mrefu mamlaka mbalimbali za serikali zimekuwa zikijitahidi kutatua migogoro hiyo lakini imekuwa haiishi na wananchi kuendelea kulalamikia.
Amesema kwa uchunguzi uliofanywa na mkoa walibaini malalamiko mengi ni ya fidia na watu walioahidiwa kupewa viwanja mbadala.
“Kimsingi maelekezo mbalimbali yalikuwa yanatolewa ili kutafuta ufumbuzi wa suala hili lakini suluhu ilikuwa haipatikani kwa kuwa halmashauri ya jiji ilikuwa haitoi kipaumbele katika kutenga fedha kwa ajili ya kulipa fidia ikiwa ni pamoja na kupima viwanja kwa ajili ya kutoa kama mbadala wa kumaliza kero hizi”amesema
Vile vile, amesema sauti za kero hizo zimeendelea kuwa kubwa na kuwafikia viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu, Katibu Mkuu wa CCM, Mwenyekiti wa CCM Mkoa na viongozi wengine ambao pia wametaka kero hizi kupatiwa utatuzi.
Pia, amesema kwa kutambua kero hizo aliitasha kikao cha wadau wote wanaohusika katika kutatua tatizo hilo wakiwepo wataalam wote wa halmashauri ya jiji la Dodoma wakiongozwa na Mkurugenzi wa Jiji, Kamishana wa Ardhi mkoa wa Dodoma.
Amesema kwa kushirikiana na wataalam wa mkoa walijadili namna bora ya kumaliza tatizo hilo ambapo walikubaliaana kuunda timu itakayoandaa mkakati maalamu wa kumaliza shida hiyo katika Jiji la Dodoma.
“Napenda kuujulisha umma huu kuwa mnamo Julai 7, 2023 kamati hiyo imewasilisha mkakati huo ambao pamoja na hatua nyingine kama mkoa tumejipanga kuutekeleza ili kutatua migogoro ya ardhi Dodoma”alisema