Na,Saleh Lujuo-Dodoma.
Ofisi ya Taifa ya Mashtaka hapa nchini Tanzania imezindua mwongozo utakaotumika na taasisi zote zinazo husika katika kukabiliana na makosa ya utakatishaji wa fedha ,ufadhili wa ugaidi na ugaidi, lengo likiwa ni kudhibiti na kupambana na makosa hayo
Taasisi hizo ni pamoja na taasisi za uchunguzi, taasisi za usimamizi wa Sheria na taasisi nyingine za kifedha.
Akizungumza leo na waandishi wa habari mara baada kuzindua mwongozo huo , Mkurugenzi wa Mashtaka hapa nchini (DPP) Sylvester Mwakitalu amesema , maendeleo ya sayansi na teknolojia yamewarahisishia wahalifu kufanya makosa mbalimbali bila kutambulika, hivyo utasaidia kudhibiti uhalifu.
"Mashirikiano ya taasisi hizi ni zile taasisi za uchunguzi,taasisi za usimamizi wa Sheria na taasisi zingine za kifedha. Mwongozo utaziongoza taasisi hizi na zitaratibiwa vizuri." Amesema Mwakitalu.
"Na taarifa za uhalifu zitakazopatikana zitapelekwa kwenye chombo kingine ambacho chenye Mamlaka ya kuweza kuzishughulikia, kuzichunguza na namna ambavyo zitafika kwenye hatua ya mashtaka. Kama makosa hayo yatathibitika kwamba upo ushahidi wa kutosha wa kuyaendesha mahakamani." ameongeza.
Aidha, Mwakitalu amesema taasisi zinapaswa kushirikiana ili mhalifu anapofanya kosa asije akatoka bila kuguswa na mkono wa sheria.
"Makosa haya yapo na tunazo kesi nyingi Mahakamani ambazo zipo zinaendelea katika hatua mbalimbali. Na wapo watu ambao tunawashtaki kwa makosa ya utakatishaji fedha, lakini pia tunazo kesi za ugaidi zinaendelea katika hatua mbalimbali mahakamani". amesema.
Kwa upande wa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya hapa nchini Aretas Lyimo, amesema madawa ya kulevya ni eneo moja wapo ambalo linatumika sana katika utakatishaji Fedha na Ufadhili wa Ugaidi, mwongozo utasaidia kuunganisha nguvu ya pamoja katika kupambana na Uhalifu.
"Mwongozo huu utatusaidia sana kupunguza makosa mbalimbali ya kihalifu hususani makosa ya kupangwa, ambayo taasisi zetu zinashirikiana katika kuyafanyia kazi". amesema Lyimo.
Utakatishaji fedha, Ugaidi na Ufadhili wa Ugaidi ni maeneo ambayo serikali inaenda kuyadhibiti ili taifa liendelee kuwa salama kwa watu wake.