EWURA YATOA ELIMU KWA MADIWANI WA JIJI LA DODOMA KUHUSU UMUHIMU WA MATUMIZI YA VYANZO MBADALA VYA MAJI.

Na,Saleh Lujuo-Dodoma.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema jitihada kubwa zinahitajika kukabiliana na upungufu wa maji katika Jiji la Dodoma ili kukidhi mahitaji ya huduma ya maji kwa wakazi wa Dodoma ikiwemo kuhamasisha matumizi ya vyanzo mbadala vya maji kama uvunaji wa maji ya mvua.

Akizungumza katika Ufunguzi Wa Mkutano Kwa Madiwani Wa jiji la Dodoma kuhusu umuhimu Wa Matumizi ya vyanzo vya Maji Mbadala Jijini Dodoma Leo Mei 12,2023 Mwakilishi Wa  Mkurugenzi Mkuu Wa Mamlaka hiyo  Eng.exaud Fatael Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) amesema pamoja na hatua ambazo EWURA imeendelea kuchukua, hali ya upatikanaji wa maji jijini Dodoma, imekuwa si ya kuridhisha na kwamba Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa sasa ina vyanzo vya maji vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita miliomi 67.1 kwa siku wakati mahitaji ya maji kwa siku ni lita milioni 133.844.

“Hii inapelekea upungufu wa lita milioni 66.744 ya mahitaji ya maji kwa siku. Hata hivyo asilimia 28 ya maji yanayozalishwa hupotea. Kutokana na upungufu huo na maji yanayopotea, huduma ya maji inapatikana kwa wastani wa saa 10 tu kwa siku,”amesema Mhandisi Fatael.

Aidha amesema kuwa vyanzo vya maji katika Jiji la Dodoma ni visima virefu ambavyo uzalishaji wake hautoshelezi mahitaji hivyo maji hutolewa kwa mgao kwa wastani wa saa 12 kwa siku.

Mhandisi Fatael,amesema kuwa  utekelezaji wa suala hilo unahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali kama Mamlaka za Serikali za Mtaa katika kutafuta suluhu ya kuimarisha hali ya huduma ya maji.

“Madiwani wanayo nafasi ya kutunga sheria ndogo ndogo, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wake na kutoa elimu, inatoa rai kwenu, madiwani, kutoa hamasa kwa wananchi mnaowasimamia katika maeneo yenu, kuweka mikakati ya kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua, wakati hatua mbalimbali za kuimarisha huduma ya maji zikiendelea kuchukuliwa na DUWASA,”amesema.

Awali Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Prof Davis Mwamfupe,amesema kuwa Jiji litahakikisha linatumia elimu hiyo ya EWURA ili wananchi kuona thamani ya kila tone la maji na kuyavuna.

''Sisi kama Madiwani wa jiji la Dodoma tunawapongeza EWURA kwa kutoa semina hiyo na tunawaahidi kuwa tutaenda kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuona thamani ya kila tone la maji na kuyavuna''amesema Prof.Mwamfupe.

Ikumbukwe kuwa Uvunaji wa maji ya mvua ni moja ya suluhisho bora kwa uhaba wa maji na usalama wa maji ambapo Uvunaji wa maji ya mvua ni teknolojia inayotumika kukusanya na kuhifadhi maji ya mvua kutoka juu ya paa, ardhi au vyanzo vya miamba kwa kutumia mbinu mbalimbali kama vile mitungi, matenki, mabwawa na vifaa vingine. 



Post a Comment

Previous Post Next Post