VISASILI NA VISAKALE KUTUMIKA KWENYE TAMASHA LA TATU LA UTAMADUNI LA KITAIFA
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imewasisitiza watanzania kushiriki Tamasha la tatu la Utamaduni la Kitaifa, ambalo litafanyika Mkoani Ruvuma, Manispaa ya Songea likiwa na dhumuni ya kuenzi na kulinda utamaduni pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia ukuzaji wa sekta za ubunifu na utamaduni.
Msisitizo huo ameutoa Katibu mkuu wizara ya utamaduni, sanaa na michezo Gerson Msigwa wakati akizungumza na WAANDISHI wa Habari leo jijini Dodoma kuelekea Tamasha la tatu la utamaduni la Kitaifa ambapo litafanyika kuanzia Tarehe 20 hadi 23 septemba 2024.
Msigwa amesema tamasha la tatu la utamaduni la Kitaifa Kwa mwaka 2024 ni Kutokana na Maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufungamanisha utamaduni na utalii, utamaduni na Biashara pamoja na utamaduni na uchumi.
Aidha,Tamasha hilo litafunguliwa na Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Septemba 20, 2024 huku kilele cha tamasha hilo kufanyika tarehe 23 Septemba, 2024 ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Tamasha hili limekuwa na faida nyingi kwa jamii ambazo ni pamoja na kuenzi utamaduni wetu, kuimarisha utangamano wa kitaifa, kuitangaza nchi yetu, kutangaza vivutio vya kiutalii na kiutamaduni, fursa za kiuchumi, na kijamii, kutanua wigo na mitandao ya kibiashara kwa bidhaa zinazozalishwa nchini hususani bidhaa za utamaduni, sanaa, na ubunifu". Amesema Msigwa
Kadhalika,Msigwa amesema tamasha hilo pia ni kuwaunganisha pamoja wadau na viongozi wa sekta katika kuendeleza na kuenzi urithi wa utamaduni na kutoa fursa ya majadiliano ya kitaaluma baina ya wananchi wa kila mkoa pamoja na kutumia utamaduni na ubunifu kama nyenzo ya kuenzi na kukuza utambulisho wa Taifa na kutangaza fursa na rasilimali zilizopo nchini.
"Tamasha la mwaka huu litakuwa na vionjo mahsusi ikiwemo mirindimo ya kiasili, kuanzia mavazi, maonesho, visasili na visakale". Amesema
Sambamba na hayo Msigwa amesema Tamasha litakuwa na mdahalo wa kitaifa utakaozungumzia mapambano dhidi ya viashiria vya mmomonyoko wa maadili na nini mchango wa jamii katika kupunguza na hatimaye kuondoa viashirika hivyo.
"Tamasha litakuwa na onesho maalumu la matumizi ya kanga ikiwa ni vazi la utamaduni wa Mtanzania".
"Tamasha litakuwa na zaidi ya vikundi 25 kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar; vikundi hivyo ni vya sanaa ya asili, ubunifu, utamaduni na mziki wa kizazi kipya".
"Tamasha litakuwa na mashindano ya uhifadhi wa ngoma za asili kwa vikundi 25 vya Tanzania Bara na visiwani"
"Tamasha litakuwa na kliniki ya Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo".
"Kutokana na umuhimu na mvuto wa tamasha hili, naomba na kuwahakikishia kampuni zote, mashirika, asasi na taasisi zinazotoa huduma mbalimbali, washirika wa maendeleo na wadau kwa ujumla kujitokeza kudhamini tamasha hili".
Kaulimbiu ya tamasha la tatu la Utamaduni la Kitaifa kwa mwaka 2024 ni ‘Utamaduni wetu ni utu wetu, tuuenzi na kuuendeleza, Kazi iendelee.