WABUNGE WAPEWA SEMINA SERA MPYA YA JINSIA


WABUNGE WAPEWA SEMINA SERA MPYA YA JINSIA

Na,Saleh Lujuo-Dodoma

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Azzan Zungu amesema ili kwenda sambamba na utekelezaji wa dhana ya kuwa na Bajeti yenye mtazamo wa kijinsia ni lazima kutazama kanuni za Bunge kama zinakidhi ipasavyo kutekeleza dhana hiyo.

Amesema kama Kanuni hizo zitakuwa na kasoro ziboreshwe ili kuwawezesha Wabunge kushauri kuhusu Bajeti kuzingatia masuala ya Jinsia kwa minajili ya ustawi wa Taifa.

Ameyasema hayo leo Juni 08, 2024 jijini Dodoma wakati akifungua semina iliyoandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Mashirika ya UN Women na UNDP kwa lengo la kuwaelimisha wabunge juu ya Sera ya Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023 na masuala ya Bajeti yanayozingatia Jinsia.

Mhe. Zungu amesema Serikali imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali katika kuhakikisha Bajeti ya Serikali na Taasisi zake zinazingatia masuala ya Jinsia ikiwemo kushirikisha wadau katika uandaaji na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali yenye kuzingatia mtazamo wa kijinsia.

Amezitaja jitihada nyingine za Serikali ni kutenga mikopo ya wanawake na makundi maalum katika bajeti za halmashauri hapa nchini ili kuongeza ushiriki wa wanawake na makundi maalum katika kujiletea maendeleo yao pamoja na ya taifa kwa ujumla. 

"Naomba nichukue fursa hii pia, kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha dhana hii ya Bajeti inayozingatia Jinsia" ameeleza Mhe. Zungu 

"Naomba nitoe rai kwa wabunge kuzingatia Semina hii ili tuweze kupata maarifa waliyotuandalia na hatimaye kutusaidia kujadili na  kupitisha Bajeti zijazo  kwa jicho la kijinsia. Hii itawezesha kufanikisha  mkakati  wa Serikali yetu wa  kuhakikisha rasilimali za umma tunazozigawa  na kuzisimamia zinawanufaisha Watanzania wote." amesisitiza Mhe. Zungu

Akizungumza katika semina hiyo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Wizara ilifanya mapitio ya iliyokuwa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000 kwa lengo la kuboresha Sera hiyo kukidhi na kuendana na mahitaji ya sasa ya jamii ya kukuza usawa wa kijinsia katika masuala kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Ameongeza kwa sasa ipo Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023 iliyozinduliwa tarehe 8 Machi, 2024 na Wizara kwa kutambua umuhimu wa Sera hii imeona ni muhimu kuwapitisha Wabunge waweze kuilewa kwa kuwa wana mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.

"Pamoja na Sera tutaelimishwa pia kuhusu umuhimu wa uzingatiaji wa Bajeti ya mrengo wa kijinsia ili katika utekelezaji wa majukumu yetu tuweze pia kuwa na jicho la kijinsia" amesema Waziri Dkt. Gwajima   

Akiwasilisha kwa wabunge kuhusu Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023 Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Seif Shekelaghe amesema uwepo wa Sera hiyo imetokana na baadhi ya mapungufu ya utekelezaji wa Sera iliyopita hivyo kutoendana na wakati uliopo.

Ameyataja miongoni mwa mapungufu hayo ni kukosekana kwa Matamko ya Kisera kwa masuala ya kijinsia yaliyojitokeza baada ya mwaka 2000, kutojumuishwa kwa baadhi ya masuala ya msingi ikiwemo ukatili wa mtandaoni na takwimu zenye mlengo wa kijinsia, Sera kutotilia mkazo eneo la mila na desturi kandamizi zinazowanyima wanawake fursa ya kumiliki na kutumia rasilimali, kutojumuishwa kwa baadhi ya Mipango, Mikataba na Itifaki za Kimataifa na Kikanda zinazohusu masuala ya usawa ya jinsia zilizoridhiwa baada ya mwaka 2000.

Ameyataja mapungufu mengine kuwa ni kutoshirikishwa kwa wanaume katika jitihada za kuleta usawa wa kijinsia na baadhi ya masuala mtambuka kutojumuishwa, hususan suala la jinsia na utawala bora.

Aidha amesema Sera mpya imelenga kukuza usawa wa kijinsia katika upatikanaji wa fursa za kiuchumi na mitaji, kutokomeza aina zote za ukatili wa kijinsia ikiwemo ule wa mitandaoni, kuwa na jamii inayoheshimu usawa na haki kwa wote, kuimarisha ushiriki wa wanawake katika ngazi za uongozi na maamuzi, kukuza usawa wa kijinsia katika upatikanaji wa elimu bora na mafunzo.

Malengo mengine ni kuboresha huduma za afya jumuishi kwa wanawake na wanaume, kuimarisha matumizi ya teknolojia katika uwezeshaji wa wanawake, kuimarisha mifumo ya ukusanyaji, utunzaji na utumiaji wa takwimu za kijinsia, kuzingatia masuala ya programu za wanawake amani na usalama, kuhimiza uzingatiaji wa huduma na kujikinga na maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI na kukuza uzingatiaji wa masuala ya kijinsia katika usimamizi wa mazingira.

Post a Comment

Previous Post Next Post