WAZAZI TENGENI BAJETI YA KUWANUNULIA TAULO ZA KIKE WATOTO WENU



WAZAZI TENGENI BAJETI YA KUWANUNULIA TAULO ZA KIKE WATOTO WENU

Na, Wizara ya Afya-ARUSHA 

Wazazi na walenzi  nchini wametatakiwa kuhakikisha  wanawawezesha watoto wa kike  kila mwezi kupata vifaa vyao vya kujilinda na kuwa na hedhi salama katika muda husika.

Rai hiyo imetolewa leo Mei 28, 2024 na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Molel wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya juma la hedhi Salama Duniani ambayo Kitaifa yameadhimishwa Jijini Arusha.

Wazazi mara nyingi tumekuwa tukitenga bajeti ya kununua vitu mbalimbali kwa ajili ya matumizi majumbani kwetu lakini eneo hili la kununua pedi ‘taulo za kike’ mara nyingi tunakuwa tunalisahau, niwaombe Wazazi na walezi wote tutenge bajeti ya kila mwezi kwa ajili ya kuwezesha hawa mabinti zetu waweze kuwa na uhakika wa kuwa na taulo za kike na kufikia malengo ya hedhi salama” amesema Naibu Waziri Dkt. Mollel.

Dkt Molel amesema Serikali imekuwa ikihimiza uwekezaji wa uzalishaji bidhaa za hedhi nchini ili ziweze kupatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu. Hata hivyo amepongeza mchango wa wadau wa Sekta katika kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa taulo hizo.

"Napenda kutoa pongezi kwa Kiwanda cha A-Z kilichopo hapa Arusha kwa kuanzisha uzalishaji wa bidhaa hizi muhimu nchini ambapo kwa sasa wanazalisha taulo za kike zitakazo weza kutumika kwa muda mrefu,"amesema Dk Mollel huku akiwaomba wazalishaji wengine  kujitokeze kuwekeza kwenye uzalishaji wa bidhaa za hedhi ili ziweze kupatikana kwa wingi na kwa gharama nafuu nchini. 

Akisoma taarifa ya Jukwaa la Hedhi Salama nchini Bi. Mariam Mashimba ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa hilo amesema hivi sasa watumiaji wengi katika shule wanapendelea taulo zakufua. 

"Wakati wa utafiti asilimia 75% ya wanafunzi waliohojiwa katika baadhi ya shule za sekondari na msingi ndani ya mikoa 22 ambako utafiti ulifanyika walionesha kupendelea zaidi taulo za kufua kwani huokoa uchumi wa wazazi wao na kutunza mazingira lakini pia huondokana na adha ya kukosa mahali pa kutupa pindi wanapomaliza kutumia" amesema Bi Mashimba.

Naye Mwakilishi wa Mkoa wa Arusha Dkt. Omary Chande, akitoa Salaam za mkoa, amesema mkoa  wa Arusha ni miongoni mikoa iliyopokea fedha nyingi kwa ajili yakutekeleza afua za afya

"Katika mwaka wa fedha 2023/24 mkoa.ulipokea zaidi ya Bil. 33.2 za uboreshaji wa miundombinu ikiwepo Hospitali ya Mkoa, Wilaya na Vituo vya Afya." Amesema Dkt. Chande

Juma la Hedhi salama ambalo lilianza Mei 25, 2024 na kuongozwa na Kaulimbiu "Kwa pamoja Tuweke Mazingira Rafiki na Endelevu kwa Hedhi Salama" limefikia mwisho leo kwenye viwanja vya Makumbusho ya Mnara wa Mwenge jijini Arusha.

Post a Comment

Previous Post Next Post