WAZIMBABWE WATUA NCHINI KUJIFUNZA MFUMO WA NeST.
Na,Mwandishi wetu
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma ya Zimbabwe (PRAZ) imeingia nchini kupata uzoefu wa uendeshaji wa michakato ya Ununuzi wa umma kupitia PPRA.
Akizungumza jana Aprili 13, 2024 baada ya kuwasili Uwanja wa ndege wa Dodoma Afisa Mtendaji Mkuu wa PRAZ Bw. Clever Ruswa amesema kuwa licha ya ziara hiyo kuwa ya muda mfupi lakini itatosha kujifunza na kubadilishana uzoefu wa uendeshaji wa masuala ya Ununuzi wa Umma baina ya Zimbabwe na Tanzania.
Bw. Ruswa amesema kuwa kilichowavutia zaidi Nchini Tanzania ni mafanikio ya ujenzi wa mfumo wa ununuzi kielektroniki uliojengwa na wataalamu wazawa suala ambalo kwake ameliita kuwa ni uthubutu wa hali ya juu kwa Serikali ya Tanzania.
“ Kitu kikubwa ambacho Zimbabwe wanaona kuwa ni mafanikio kwa Serikali ya Tanzania ni kuwa na mfumo wa kielektoniki wa ununuzi amabao umejengwa na wataalamu wa kitanzania, hakika huu ni uthubutu wa hali ya juu. Alisema Bw. Ruswa.
Sambamba na hilo Bwa. Ruswa ameweka wazi matarajio ya ziara yao hiyo kuwa hawategemei kutoka patupu badala yake watapata mambo mengi mazuri ya kujifunza kupitia PPRA ikiwa ni pamoja na namna ya kupata ufanisi katika ununuzi wa Umma kupitia mfumo wa NeST ambao unatumika na PPRA katika kuendesha michakato ya utoaji wa zabuni za umma.
Mfumo wa NeST umeanza kutumika rasmi mwezi Julai 2023 ambapo mpaka leo Aprili 14, 2024 Jumla ya mikataba ya zabuni 12320 yenye thamani ya TSH Trilioni 3.35 tayari imeshatolewa.