REA IMEANZA KUTEKELEZA PROGRAM YA KUSAMBAZA GESI ASILI VIJIJINI



REA IMEANZA KUTEKELEZA PROGRAM YA KUSAMBAZA GESI ASILI VIJIJINI

Na,Saleh Lujuo-Dodoma

katika kutekeleza ajenda ya matumizi ya Nishati safi ya kupikia,REA kwa mwaka huu wa fedha wa 2023/2024, imetoa zaidi ya mitungi ya gesi ya kupikia 158,100 kwa Wananchi wa vijijini kama sehemu ya hamasa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na mitungi zaidi ya laki 4 itatolewa kupitia utaratibu huo.

hatua hiyo ni kuunga mkono Jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika matumizi ya Nishati safi ya kupikia ili kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanaleta athari kubwa kwa jamii.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Mbadala na Jadidifu, Mhandisi, Advera Mwijage leo, Tarehe 9 Machi, 2024 jijini Dodoma katika Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia ambalo limekwenda sambamba na kuhitimisha Maadhimiho ya Siku ya Wanawake Duniani (2024).

Aidha,Mhandisi Advera,amesema mbali na ugawaji wa mitungi ya gesi, REA imeanza kutekeleza program ya kusambaza gesi asili kwa Wananchi wa vijijini wa mkoa wa Pwani na Lindi.

"Tumeanza kutekeleza program ya kusambaza gesi asili Kwa wananchi na Mradi huo una thamani ya shilingi bilioni 6.8 ambapo kwa kuanzia kaya zaidi 980 zitaunganishwa kwenye mtandao wa gesi asilia kwenye nyumba zao". Amesema

Sambamba na hayo Mhandisi Advera ameutaja Mradi mwengine ni wa kuwaunganisha Wananchi wa vijijini katika mkoa wa Pwani na Mtwara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Mradi huu una thamani ya shilingi bilioni 13.5 ambapo kwa kuanzia kaya zaidi ya 1,400 zitanufaika.

Pamoja na hayo Mhandisi Advera amesema REA pia inatekeleza Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza, ambapo Tanzania kuna magereza zaidi ya 129.

 "Tumeambiwa kwamba matumizi ya kuni pekee yake ni zaidi ya asilimi 93,na kiukweli ni uharibifu mkubwa sana wa kimazingira na tumeanza Sasa   kutekeleza mradi huo na utagharimu shilingi bilioni 40". Amesema

REA inatekeleza jukumu la kuhakikisha nishati za aina zote zinapatikana vijijini na kwa Watu wote na itaendelea kuwa mstari wa mbele kuwasaidia Waendelezaji wa teknolojia za nishati safi pamoja na Miradi inayolenga kwenye kuongeza upatikanaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia.

Kongamano la wanawake la kugawa mitaji na vitendea kazi vya Nishati safi ya kupikia limebebwa na ujumbe usemayo,Nishati safi ya kupikia Mkombozi kwa wanawake.

Post a Comment

Previous Post Next Post