RAIS SAMIA KUWAONGOZA VIONGOZI IBADA YA KUMBUKIZI YA MIAKA 40 YA KIFO CHA SOKOINE
Na,Saleh Lujuo-DODOMA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwaongoza viongozi mbalimbali kwenye ibada maalum ya kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa tatu wa Tanzania katika kipindi cha awamu ya Kwanza.
Ibada hiyo itakayofanyika siku ya Ijumaa Aprili 12, 2024, saa 3:00 asubuhi, imeandaliwa na familia ikishirikiana na Taasisi ya Hayati Edward Moringe Sokoine.
Hayo yameelezwa leo Marchi 28,2024 jijini Dodoma na Msemaji wa Familia hiyo Lembris Marangushi Kipuyo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amemtaja Hayati Sokoine kuwa alikuwa mzalendo wa kweli, aliyependa taifa lake na wananchi wake kwa kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika na watanzania wote.
Ikumbukwe kuwa hayati Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vipindi viwili wakati wa uongozi wa Awamu ya Kwanza. Alizaliwa Agosti 01, 1934, kijijini Enguik, Monduli Juu wilayani Monduli, mkoani Arusha.