HATUWEZI KUITENGANISHA TAMISEMI NA WAKANDARASI WAZAWA-WAZIRI MCHENGERWA



HATUWEZI KUITENGANISHA TAMISEMI NA WAKANDARASI WAZAWA-WAZIRI MCHENGERWA 

Na,Saleh Lujuo-DODOMA

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa ameitaka 
Wakala ya barabara za vijijini na Mijini (TARURA) kujipanga kuwawezesha wakandarasi wazawa ili wawe na uwezo wa kushindana kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Mhe.  Mchengerwa Kwenye Kikao kazi chake na watumishi wa wakala ya barabara za vijijini na Mijini (TARURA) ambapo amesema maagizo hayo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"TARURA  wakuzeni na kuwaendeleza wakandarasi wazawa ili watoe mchango mkubwa kwa Taifa na washindane kimataifa". amesisitiza 

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka watendaji wa TARURA wa Mikoa na wilaya kusimamia kazi kwa weledi na kuzingatia masharti ya Mikataba ili kazi zikamilike kwa viwango vilivyo ainishwa kimkataba.

Sambamba na hayo,ameipongeza TARURA kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ya mawe (cobble stone roads) na madaraja ya mawe (stone arch bridges) na majaribio ya teknolojia nyingine katika kuboresha barabara wanazosimamia.

"Tangu kuanzishwa kwa wakala huyo mwaka 2017 kumekuwa na ongezeko la barabara Za lami kutoka kilomita 1,449.55 hadi kilomita 3,053.26 sawa na ongezeko la  110% pia barabara za changarawe zimeongezeka kutoka kilomita 24,405.40 hadi kilomita 38,141.21 sawa na ongezeko lake la 56%". Amesema.

Naye,Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema wataendelea kufanya kazi ili kutimiza malengo ya TARURA pamoja kuwakuza wakandarasi wazawa Kwa kushirikiana na bodi ya wakandarasi nchini pamoja na taasisi za kifedha.

Kikao kazi cha waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI) na watumishi wa wakala ya barabara za vijijini na Mijini (TARURA) dhamira yake ni kuhakikisha miundombinu yote ya barabara inatekelezwa Kwa viwango vya Juu.




Post a Comment

Previous Post Next Post