WANAOJIHUSISHA NA VITENDO VYA KUTOA NGUZO ZA MAJINA YA ANWANI ZA MAKAZI KATIKA BARABARA, WAACHE MARA MOJA VITENDO HIVYO-DC SHEKIMWERI
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabiri Shekimweri, amesisitiza kuundwa kwa Timu ya ufuatiliaji na tathmini ya zoezi la Anwani za Makazi ili kufanikisha azma ya Serikali ya kila Mtu kutambulika kirahisi mahali anapoishi kwa lengo la kufikiwa na huduma za Kijamii kwa haraka.
Aidha,ametoa Rai kwa wanaojuhusisha na vitendo vya kung'oa nguzo za Majina ya Anwani za makazi Katika barabara waache mara Moja vitendo hivyo kwani serikali haitosita kumchukulia hatua kali yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo vyenye nia ovu.
Shekimweri amesisitiza hayo leo Jijini Dodoma ,wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya Kuwajengea uwezo kuhusu Mfumo wa anwani za makazi kwa Maafisa Tarafa,Maafisa Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Maafisa Watendaji wa Mitaa wa Jiji la Dodomaa.
"Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wananchi kuharibu nguzo za majina barabarani, natoa rai kwa yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja na sisi kama Serikali hatutasita kumchukulia hatua kali yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo vyenye nia ovu". Amesisitiza
Aidha, Shekimweri amesema kuwa Anwani ya makazi ni hitaji la msingi katika kuwezesha ukuaji wa sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi na ni Nyenzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali ambao ndio umeshika kasi katika ulimwengu wa sasa.
Amesema Jiji la Dodoma ni miongoni mwa miji inayokuwa kwa kasi sambamba na kuwa na ongezeko kubwa la watu ambapo Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2022, Jiji la Dodoma lina watu wapatao 765,179 na Kaya zipatazo 214,330.
" Hali hii inapelekea ongezeko kubwa la upimaji wa maeneo na ujenzi wa makazi mapya ambayo yanahitaji kutambuliwa na kupatiwa Anwani za Makazi pamoja na Kasi ya ukuaji wa Jiji letu inapaswa kwenda sambamba na kasi ya utambuzi na utoaji wa Anwani za Makazi". Amesema
"sisi tutakaopatiwa mafunzo tufahamu kwamba tunahitaji kwenda kuongeza kasi ya utoaji wa Anwani za Makazi". Ameongeza
Kwa Upande wake Mratibu wa anwani za Makazi Kitaifa,Mhandidi Jampion Mbugi, amesema Matarajio ya Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ni kuona Jiji la Dodoma linakuwa la Mfano katika utekelezaji na matumizi ya Anwani za Makazi na kuwa chachu kwa Halmashauri nyingine kuja Dodoma kujifunza namna ya kufanikisha utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi.
"Na hii ndio dhamira ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika kutekeleza Mfumo wa Anwani za Makazi na Utekelezaji wa Mfumo huu ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025, Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Malengo ya Dunia ya Maendeleo Endelevu hususan lengo la 8 na 9 ambayo yote kwa pamoja yanalenga kuboresha maisha ya wananchi". Amesema.
Akitoa wasilisho kwa Maafisa Taarafa, wenyeviti na Watendaji wa kata na Miata wa Halmashauri ya Ia jiji la Dodoma, Afisa Ardhi wa wizara ya Ardhi nyumba na maendeleo ya Makazi Anorld Mkude amesema kuwa Anuani za Makazi zinamanufaa makubwa Katika kuiwezesha Mipango na Tafiti Kufanyika kwa Tija pamoja na Kuimarisha Ulinzi na usalama.
"Sote tunatambua kwamba suala la utekelezaji wa anwani za makazi ni maelekezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo aliyotoa siku anazindua “Operesheni anwani za makazi”. maelekezo yale hayakuishia kwenye operesheni pekee bali alielekeza tuendelee kuwapatia Watanzania anwani za makazi ili tuweze kutambuana kwa urahisi “Nani ni Nani na Anaishi wapi”. Amesema.
Julius Magawa Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Mkoyo Kata ya Hombolo Bwawani amesema wao kama watendaji wataendelea kusimamia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha dhamira yake ya dhati ya kuleta maendeleo kwa wananchi inafikiwa.
Mafunzo Hayo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Maafisa Taarafa, wenyeviti na Watendaji wa kata na Miata wa Halmashauri ya Ia jiji la Dodoma kuhusu Anwani za Makazi yameandaliwa na wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Lengo la kuhakikisha kila mwananchi anatambulika kwa kutumia Anwani ya Makazi ili kuboresha mfumo wa maisha ya Watanzania na kuimarisha ufikishaji wa huduma
Tags:
Habari