TUMIENI MBINU MBADALA KUKAMILISHA UJENZI WA MIRADI KWA WAKATI RC-SENYAMULE
Na,Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amewataka mafundi wa Shule Mpya ya Sekondari Manchali inayojengwa kupitia fedha za Mradi wa Sequip na Shule ya wasichana ya Mkoa wa Dodoma inayojengwa katika Kijiji cha Manchali Wilayani Chamwino kukamilisha Ujenzi wa Miradi yote kwa wakati uliopangwa na kuzingatia ubora unaokubalika.
Mhe. Senyamule ametoa maagizo hayo Septemba 14, 2023 katika ziara yake ya kikazi ya kukagua Miradi mbalimbali ya Ujenzi wa chuo cha Veta, Shule za Sekondari na kuongea na kusikiliza kero za wananchi wa kata ya Mlowa barabarani kupitia Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mlowa Barabarani.
"Msije mkasema inashindikana kukamilisha Mradi kwa wakati tumieni njia mbadala ili mkamilishe, nyie mafundi ni wataalamu angalieni njia nzuri ya kufanya kazi mbili kwa wakati mmoja lakini kwa kuzingatia ubora unaotakiwa na ikiwezekana ongezeni muda wa kufanya kazi na hakikisheni vifaa vyote vimenunuliwa ili kurahisisha Ujenzi", Amesema Senyamule.
Aidha Senyamule amewaasa wananchi wa Manchali kuchangamkia fursa zinazojitokeza kutokana na Ujenzi huo kwani kutakuwa na mahitaji mbalimbali kutokana na ujio wa wanafunzi, Walimu na wageni tofauti tofauti watakaokuja katika Shule hizo.
"Mkoa wa Dodoma unajumla ya kata 209 na kata yenu imepata bahati ya Miradi miwili mikubwa sasa changamkieni fursa kwasababu kutahitajika vyakula hapa na ujio wa wageni watahitaji mahali pakuishi kwahiyo changamkeni ujio wa Miradi hii kupata fursa za kujiingizia kipato", Mhe. Senyamule
Ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kikazi Mkoani hapa Mhe. Senyamule amekagua Ujenzi wa Shule Mpya ya Kata ya Manchali, Mradi wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Dodoma, Chuo cha Veta pamoja kuongea na wananchi wa kata ya Mlowa barabara ambapo amewaasa wananchi wa Kijiji hicho kuwa na umoja ili kurahisisha ufanisi wa utekelezaji wa Miradi ya maendeleo ya Kijiji hicho ikiwemo upatikanaji wa Maji Safi na salama.