SERIKALI IMEPIGA MARUFUKU UINGIZAJI WA MAJOKOFU YA MTUMBA NCHINI
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Serikali imepiga marufuku uingizaji wa Majokofu ya Mtumba pamoja na viyoyonzi ambavyo vinatumia Gesi vimekuwa na madhara ya uharibifu wa tabaka la ozoni ambalo limekuwa na athari kwa Afya za wananchi ikiwemo mabadiliko ya tabianchi.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,DK Seleman Jaffo wakati akitoa taarifa kuhusu maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uhifadhi wa tabaka la ozoni kuhusu kemikali zinazomomonyoa tabaka la ozoni ambayo yatafanyika Septemba 16 Mwaka huu.
"tabaka la ozoni linapoharibiwa husababisha saratani ya ngozi, mtoto wa jicho, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi, kujikunja kwa ngozi, kuathirika kwa ukuaji wa mimea pamoja na kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi". Amesema Dkt. Jaffo
Dkt. Jaffo ametaja madhara ya kemikali hizo ikiwemo kuathirika kwa ukuaji wa mimea pamoja na kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi.
“Ukiangalia mwaka juzi (2021) kuna kazi mbalimbali zilikuwa zikifanyika kwa mafundi wa majokofu pamoja na kutembelea maduka ili kuhamasisha na kutoa mafunzo kwa mafundi ili waweze kutambua madhara yake na kuchukua hatua,” amesema Dkt. Jaffo.
Katika hatua nyingine, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imempongeza Rais Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia suluhu Hassan kuteuliwa Rasmi kuwa mjumbe wa Bodi ya ushauri ya kituo cha dunia cha Uhimilivu wa mabadiliko ya Tabianchi (GCA).
Maadhimisho ya siku ya uhifadhi wa tabaka la ozon yanaenda sambamba na Kaulimbiu isemayo "itifaki ya Montreal hifadhi ya tabaka la ozoni na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi".
Ikumbukwe kuwa Ozoni ni tabaka la hewa lililopo kwenye angahewa ya juu umbali wa takribani kilometa 15 hadi 30 juu ya Ardhi likiwa na kazi ya kuchuja kiwango cha mionzi isifike katika uso wa Dunia.