EWURA YAVIFUNGIA VITUO VIWILI VYA MAFUTA KWA KUKIUKA SHERIA
Na,Saleh Lujuo-Dodoma
Mamlaka ya udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imevifungia Vituo vingine viwili vya Mafuta vya Mkoa wa Morogoro na Manyara kwa muda wa miezi sita baada ya kujiridhisha pasipo shaka kuwa vituo hivyo vinahodhi mafuta kwa lengo la kupata maslahi ya kibiashara ikiwemo faida kubwa kinyume na Sheria.
Meneja Mawasiliano na uhusiano EWURA Titus Kaguo amesema hayo Leo Jijini Dodoma wakati akitoa Taarifa kwa Waandishi wa Habari kuhusu muendelezo wa Uchunguzi wa Vituo vingine ikiwemo kuwapa fursa ya kuwasilisha utetezi wao ndani ya siku 21.
Amebainisha kuwa baada ya kupitia utetezi wao katika kikao cha tarehe 29 Septemba Mwaka 2023 Bodi ya Wakurugenzi EWURA ilijiridhisha pasipo shaka kuwa vituo vingine viwili vya Rashal petroleum LTD kilichopo Mlimba Mkoani Morogoro na Kimashuku investment Co.ltd kilichopo Babati Mkoani Manyara vilihodhi Mafuta kati ya Mwezi julai na Agosti 2023 kinyume na sheria.
"Kama Mamlaka tuliamua kuvifungia vituo hivi Kwa muda wa miezi Sita kutokana na kukiuka kanuni na sheria ambazo haziendani na matakwa ya Nchi Juu ya uuzaji wa Biashara ya mafuta". Amesema
Pamoja na hayo ,EWURA imewataka Wafanyabiashara wote wa Mafauta pamoja na wamiliki kufuata Sheria kanuni na Miongozo inayosimamia Biashara ya mafuta nchini.
Katika hatua nyingine Meneja huyo ametoa onyo kwa wamiliki wa vituo vya Mafuta ,kuwa Serikali inafuatilia suala hilo kwa karibu na ikithibitika uvunjaji wa Sheria na kanuni umetendeka hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kufutiwa leseni.
Licha ya hayo EWURA imesema hali ya upatikanaji wa Mafuta nchini inaridhisha kutokana na mafuta kuwepo yakutosha.
Tags:
Habari