BAHI YAJIPANGA KWA UWEKEZAJI WENYE TIJA
Na,Saleh Lujuo-Dodoma.
Afisa Kilimo,Uvuvi na Mifugo Wilaya ya Bahi Siwajibu Seleman ametoa rai kwa wawekezaji wa Viwanda nchini kuwekeza Wilayani humo ili kuongeza ari ya wakulima kuzalisha zaidi na kuleta tija ya thamani ya mazao.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Aug 4,2023 kwenye maonesho ya wakulima (Nanenane)Kanda ya kati yanayoendelea Jijini Dodoma amesema njia pekee ya kuwainua wakulima ni uwepo wa Viwanda vya kutosha.
Amesema uwepo wa Viwanda Bahi utaongeza uhakika wa wakulima kulima mazao mengi na kuwa na soko la uhakika na kuondokana na hofu ya kuharibika kwa mazao yao .
"Kuna wakati wakulima wanatamani kulima zaidi lakini wanahofu kupoteza nguvu zao,njia pekee ya kuwaokoa ni kuwepo Viwanda vya usindikaji hali itakayo wainua kiuchumi na kuwa na maisha bora,"amesema
Ametaja baadhi ya maeneo ya uwekezaji kwenye Wilaya hiyo kuwa ni Ufugaji wa Ng'ombe,uvuvi,Kilimo cha mpunga, Alizeti,zabibu,mtama Pamoja na Kilimo cha mahindi.
Amesema zao la alizeti kwenye Wilaya hiyo ni la kimkakati na hivyo kupewa kipaumbele katika kuchochea biashara na uwekezaji huku zao la mtama likitiliwa mkazo kwa ajili ya chakula.
"Asilimia 70 ya wakazi wa Bahi wanajihusisha na kilimo pamoja na ufugaji,tunajivunia kuwa na Mifugo mingi kulingana na mahitaji ambapo kuna Ng'ombe zaidi ya laki tatu pamoja na mbuzi zaidi ya laki moja na nusu,"amesema
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya maendeleo ya Jamii na vijana wa Wilaya hiyo Denis Komba ameeleza kuwa Ili kufanikiwa kwenye masuala ya uwekezaji na masoko, Wilaya ya Bahi imejipanga kuwanufaisha vijana, wanawake na wenye ulemavu kulima Kilimo biashara na kuongeza thamani ya mazao.
Komba amesema kupitia maonyesho ya wakulima yanayoendelea Jijini hapa,Ofisi yake imefanya jitihada za kuyafikia makundi hayo na kuwaelimisha namna bora ya kulima kwa tija na kuzifanya za Kilimo kuwa biashara na hatimaye kupelekea kuwa ajira.
Amesema lengo ni kuwahamasisha vijana wote nchini kuwa na ari ya kuboresha bidhaa za Kilimo kuwa zenye thamani na Ubunifu zinazoenda na wakati .
"Tunawatengeneza vijana na Jamii Kwa ujumla kupitia biashara zao kupata ajira,tunataka Kila mmoja aone thamani ya Kilimo biashara kuwa ni ajira,kupitia hamasa tunayoitoa watu wataachana na kilimo cha zamani na kuanza kubadilika,"amesema
Pamoja na hayo amesema ili kuwezesha vijana kufanikiwa zaidi,Ofisi hiyo imekuwa ikitoa mikopo ya riba Nafuu Kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu wa Wilaya hiyo ili kuwasaidia lijikwamua kiuchumi.
"Tunaendelea kuwawezesha wajasiriamali kupitia vikundi vyao kwa kuwakopesha, Dunia ya Sasa inahitaji bidhaa zenye thamani ya Ubunifu na ubora ili soko la uhakika liwepo,kwa kuliona hili tayari kwa mwaka wa fedha 2022/2023 tumewawezesha watu 123 lengo ni kuwafikia watu 150,"amefafanua Komba
Zaidi ya hayo ameeleza kuwa Serikali kupitia Divisheni hiyo ina mpango wa kuwawezesha wajasiriamali hao mafunzo ya TEHAMA ili kuendana na ulimwengu wa kidigitali hali itakayo wasaidia kufanya biashara mtandao na kuwa wa kisasa zaidi.
Komba amesema tofauti na zamani mfumo wa uombaji wa mikopo wa sasa
unawahitaji wajasiriamali wawe na ujuzi wa kuomba Kwa njia ya mtandao jambo ambalo ni gumu Kwa kuwa wengi wao hawana elimu hiyo na kusababisha kuchelewesha kupata mikopo kwa wakati na kupelekea kukata tamaa
"Wajasiriamali wengi tunao wahudumia hawajui matumizi ya TEHAMA,wengi ni wa pembezoni,Dunia inatutaka tuendane na teknolojia hii hivyo kwa kuanza tumeanza kuwaelimisha Maafisa Kata kwenye Kata tano Bahi ili waweze kuwasaidia wajasiriamali kujisajili kwa ajili ya mikopo,"amefafanua
Mkuu huyo wa Divisheni ya maendeleo ya jamii ametumia nafasi hiyo pia kuwahamasisha vijana kuendelea kushiriki maonesho hayo kujifunza mbinu Mpya za uzalishaji ili kuboresha mazingira ya kilimo Kanda ya kati na hatimaye Tanzania Kwa ujumla.