𝗨𝗝𝗔𝗭𝗔𝗝𝗜 𝗡𝗔 𝗨𝗧𝗘𝗡𝗚𝗘𝗡𝗘𝗭𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗗𝗢𝗗𝗢𝗦𝗢 𝗦𝗔𝗦𝗔 𝗡𝗜 𝗞𝗜𝗗𝗜𝗝𝗜𝗧𝗔𝗟𝗜.

𝗨𝗝𝗔𝗭𝗔𝗝𝗜 𝗡𝗔 𝗨𝗧𝗘𝗡𝗚𝗘𝗡𝗘𝗭𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗗𝗢𝗗𝗢𝗦𝗢 𝗦𝗔𝗦𝗔 𝗡𝗜 𝗞𝗜𝗗𝗜𝗝𝗜𝗧𝗔𝗟𝗜.

Na,Mwandishi wetu-Dodoma.

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imefanikiwa kutengeneza mfumo shirikishi wa kidijitali wenye usalama na gharama nafuu unaomuwezesha mwananchi au taasisi kutengeneza na kujaza dodoso, kupata tathmini pamoja na takwimu za dodoso kwa njia ya mtandao. 

Meneja wa Kituo cha Utafiti na Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao (eGovRIDC) cha e-GA, Mhandisi Dkt. Jaha Mvulla ametoa kauli hiyo ofisini kwake jijini Dodoma ambapo amesema Mfumo huo ni Rafiki na shirikishi wenye usalama na gharama nafuu.

“Mamlaka tuliamua kutengeneza mfumo huu ili kuwepo na mfumo shirikishi na salama wa kuhifadhi takwimu zinazotokana na madodoso, kuzuia urudufu wa utengenezaji wa madodoso, pamoja na kupunguza gharama kutoka kwenye mifumo ya dodoso inayotumia leseni” amesema Dkt. Jaha.

Mfumo huo umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni dodoso LITE na dodoso PRO ambapo, katika utengenezaji wa maswali na upatikanaji wa takwimu katika dodoso LITE umefanywa kuwa urahisi zaidi ili kumrahisishia mtumiaji katika kujaza au kutengeneza dodoso.

Walengwa wakuu wa mfumo huu ni Taasisi za Umma na wananchi wenye uhitaji wa kutengeneza madodoso ili waweze kupata takwimu au majibu sahihi ya dodoso husika, amesema Jaha.

“Mfumo huu una uwezo wa kuhifadhi data pia ni salama kwakuwa umejengwa na wataalamu wazalendo wa ndani na unawaruhusu watumishi kufanya uchambuzi, kuhifadhi na kupata takwimu za madodoso ya taasisi yanayotengenezwa, pia taasisi au mtu binafsi anaweza kutengeneza dodoso muda wowote na mahali popote kwa jia ya mtandao” amesema Jaha.

Aidha, mtumishi anaweza kutengeneza dodoso la taasisi na kugawa namba ya dodoso na nywila kwa wahusika tu ili waweze kujaza na pia, mfumo unaruhusu na kuziwezesha taasisi kutengeneza maswali katika fomati mbalimbali na kutumia njia ya program ya simu au Kivinjari katika kujaza dodoso.

Kwa sasa Mfumo huu unapatikana bila gharama yoyote kupitia https://edodoso.gov.go.tz, ili taasisi iweze kuunganishwa na kutumia mfumo huu, taasisi husika inapaswa kuwasiliana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kupitia Dawati la Msaada http://helpdesk.ega.go.tz/.

Post a Comment

Previous Post Next Post