UHUSIANO WA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI UKO IMARA

Na Mwandishi Wetu Pretoria, Afrika Kusini 

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema uhusiano wa Tanzania na Afrika Kusini uko imara na unaendelea kukua siku hadi siku katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya Utamaduni.

Balozi Milanzi amesema hayo Mei 22, 2023 jijini Pritoria nchini Afrika Kusini wakati akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo ambao walifika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini humo kujitambulisha kuwa watakuwa kwenye ziara ya mafunzo yenye lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu na Afrika Kusini katika masuala ya Utamaduni na Sanaa.

“Ugeni huu sasa ni wa pande mbili za Muungano hasa kwenye eneo hili muhimu la Utamaduni. Utamaduni ni dhana pana zaidi, kuna suala la lugha, vyakula, mavazi. Mimi nimependa sana mwelekeo huu wa Serikali na wizara zetu za Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, sasa zinafanya vizuri kwenye masuala ya michezo, masuala na Utamaduni, karibuni sana hapa Afrika Kusini” amesema Balozi Milanzi.

Uhusiano huo mwema umedhihirishwa kwa mahusiano mazuri baina ya nchi hizo mbili ambapo baadhi ya wajumbe kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wapo Afrika Kusini kwa ziara ya mafunzo yenye lengo la kubadilishana uzoefu katika kuendesha sekta za Wizara hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa msafara ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi. Fatma Hamad Rajab amesema kuwa nchi zetu zinahitaji kushirikiana ili kutunza urithi wake kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Aidha, mafunzo hayo pamoja na mambo mengine yanalenga kubadilishana ujuzi na kuboresha namna ya kuendesha Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika ili kuhifadhi, kulinda na kuendeleza historia ya nchi hizo mbili za Tanzania na Afrika Kusini.

Post a Comment

Previous Post Next Post