Na,Saleh Lujuo Dodoma.
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imeweka wazi kukamilika kwa Rasimu ya sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 ambapo Rasimu ya Mitaala mipya ya Elimu ya Msingi,Sekondari na vyuo vya ualimu ambayo inakidhi maelekezo ya Rais nayo imekamilika.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ametoa kauli hiyo leo Mei 9.2023 jijini Dodoma ambapo Amesema serikali imeamua kutoa Rasimu hizo hadharani ili kupata Maoni ya mwisho na Maoni hayo mwisho Wa kuyapokea ni Tarehe 31 mwezi mei 2023.
"Ninayo Furaha Kuwajulisha Kuwa Rasimu ya sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 imekamilika,kadhalika Rasimu ya Mitaala mipya ya elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ualimu ambayo inakidhi maelekezo ya Rais nayo imekamilika, Sasa serikali imeamua kutoa Rasimu hizi hadharani ili kupata Maoni ya Mwisho na Maoni hayo mwisho Wa kuyapokea ni Tarehe 31 mwezi mei 2023" Amesema Prof Mkenda.
Aidha,Prof Mkenda amesema Wizara imeandaa semina na Makongamano mbalimbali ya kuwapitisha wadau katika Rasimu hizo ikiwemo semina kwa wabunge wote na kuwapitisha kwenye Rasimu hizo za mapitio ya sera na Mitaala mipya itakayofanyika Mei 10, 2023 ambapo Mei 12 -14, 2023 Kutakua na kongamano kubwa la kitaifa la kujadili Rasimu hizo litakalofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
"Wanaotaka kuhudhuria kongamano hilo wanakaribishwa kujisajili ambapo Tangazo la kualika kujisajili linaanza leo na utaratibu wa kujisajili utatangazwa lakini Wapo wataalamu na wadau mbalimbali wamepewa mwaliko Rasmi kuja na tutajitahidi kulitangaza kongamano hili ili kila mtu asikilize maoni yanavyotolewa". Amesema Prof. Mkenda
Prof Mkenda amesema kukamilika kwa Rasimu ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 na Rasimu ya Mitaala mipya ya elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ualimu ambayo inakidhi maelekezo ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni mageuzi Makubwa kutokea nchini kwenye Masuala ya Elimu.
"Maelekezo ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassani yalikuwa kazi ifanyike kwa umakini Mkubwa sana na Rasimu zitakapotoka na mtakavyosikia mjadala kutakuwa na kalenda ya utekelezaji, tunatakiwa kuanza kufanya nini Mwakani,nini kinaenda Mwaka ujao na utekelezaji utakamilika mwaka Gani, kwakweli kuna mambo makubwa na ninachoweza kuwaambia tu haya ni mageuzi Makubwa kutokea katika nchi yetu katika suala la Elimu" Amesema Mkenda.
Watanzania wametakiwa kupitia rasimu hizo na kutoa maoni yao ambapo Rasimu hizo zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia,Tovuti ya Idara ya Habari Maelezo, na Tovuti ya Taasisi ya Elimu Tanzania.